Thursday, January 21, 2010

JINSI YA KUDHIBITI MBU KATIKA MIKOROSHO






JINSI YA KUDHIBITI MBU KATIKA MIKOROSHO

1.0 Utangulizi.
Kuna aina mbili za mbu wa korosho ambao huleta uharibifu mkubwa sana katika zao la korosho, hasa katika kanda ya kusini:
♦ Mbu wa mikorosho (Helopeltis spp)
♦ Mbu wa minazi (Pseudotheraptus wayii)

1.1 Mbu wa mikorosho (Helopeltis spp)
Helopeltis ni wadudu jamii ya mbu wenye uwezo wa kuruka toka mkorosho hadi mwingine. Wadudu hawa wenye urefu wa milimita 5 - 10, wana mchanganyiko wa rangi ya njano, nyekundu na sehemu ya weusi kwenye mabawa (Picha 1). Wadudu hawa huchangamka na kurukaruka nyakati za mchana, lakini asubuhi huwa watulivu kutokana na hali ya ubaridi.
1.2. Mbu wa Minazi (Pseudotheraptus wayii)
Mbu wa minazi wanafanana na wadudu waitwao kangambili ambao ni maarufu sana kwenye pamba na sufi. Wadudu hawa wana mchanganyiko wa rangi ya udongo na nyekundu na wana urefu wa milimita 14 - 15. Wadudu hawa wakiguswa hutoa harufu kali kama njia ya kujihami. Wanafahamika vizuri kwa majina ya kilugha kama vile "Nanoli" (Kimakonde); "Nandoli" (Kimwera, Kiyao).

2.0. Mashambulizi
Aina hizi za mbu hushambulia maeneo machanga hasa majani, machipukizi, maua na tegu pia. Mbu hawa hutoboa eneo la mashambulizi kwa kutumia mwiba wa kwenye midomo yao na kwa kufanya hivyo, mate yao yenye sumu huingia ndani ya mmea. Mate yenye sumu huleteleza makovu meusi katika maeneo ya mashambulizi. Majani yaliyoshambuliwa huweza kukunjamana, hatimaye kukauka. Machipukizi na maua yanaweza kudumaa yasiendelee na ukuaji, huku yakibaki na makovu meusi. Penye mashambulizi makali ya mbu wa mikorosho, machipukizi kukauka pamoja na majani na kusababisha ugonjwa uitwao "debeki". Ukaukaji huanza nchani na kuteremkia chini ya chipukizi. Mashada ya maua yaliyoshambuliwa hushindwa kuzaa kabisa. Miti iliyoshambuliwa sana huonekana kama imebabuka na moto.
Mbu wa minazi hushambulia pia tegu na mabibo machanga na kuacha makovu meusi yenye kuzama ndani kwenye ganda. Tegu zilizoshambuliwa zikiwa changa sana, hubadilika rangi na kuwa nyeusi, husinyaa, kisha hupukutika chini. Pia baadhi ya korosho hizo huambatana na makovu.

3.0. Jinsi ya kuthibiti Mbu waharibifu.
Mbu hawa wa aina zote mbili, pamoja na wadudu wa aina nyingine nyingi, wanaweza kuthibitiwa kwa njia mbili:

3.1 Kutumia madawa
Aina mbalimbali za madawa zimefanyiwa utafiti wa kina na kuonekana kwamba dawa aina ya KARATE ni bora kwa kuangamiza wadudu wa aina nyingi. Dawa hii hupuliziwa kutumia mashine za moto (Mist blower) au za kawaida (Knapsack sprayer) kutegemeana na ukubwa wa mkorosho. Kiwango kilichopendekezwa ni kuchanganya mililita 3 - 5 za dawa kwa lita moja ya maji kwa mti mkubwa. Upuliziaji unaanza mara baada ya kuonekana mashambulizi na kurudia inapobidi. Matunda yaliyopuliziwa dawa yasitumike mpaka baada ya siku 21 (wiki 3).

3.2 Kutumia udhibiti wa kibaolojia (Biological control).
Pamoja na uwezo mkubwa wa kudhibiti na kuangamiza wadudu kwa kutumia madawa, lakini madawa ni ya gharama mno na yana madhara sana katika mazingara yetu, ikiwa ni pamoja na kuua wadudu wenye manufaa kwa mazao yetu. Kwa ajili hiyo jitihada za kiutafiti zinafanyika ili kumsaidia mkulima kupunguza uwezekano wa kutumia madawa katika mazao.
Utafiti wa kina umefanyika kuchunguza kama kuna wadudu aina nyingine ambao wanaweza kutumika kuangamiza wadudu waharibifu wa mikorosho. Hatimaye imeonekana kwamba wadudu aina ya Majimoto (Oecophylla longinoda) wanao uwezo mkubwa wa kuangamiza aina zote za mbu waharibifu wa mikorosho. Katika uchunguzi wetu, majimoto wameonekana mara nyingi tu wakikamata aina
hizi za mbu wa mikorosho na kuwakokota hadi kwenye viota vyao kwa ajili ya kufanya chakula. Baadhi ya viota vilivyowahi kufunguliwa, vimekutwa na mabaki ya sehemu ya mbalimbali za mbu hawa, kama vile mabawa, miguu, midomo n.k.
Matokeo ya majaribio yameonyesha wazi kwamba mikorosho yenye majimoto wengi haishambuliwi na mbu wa mikorosho. Majimoto wakitanda kwenye machipukizi, maua au tegu hufanya ulinzi mzuri sana dhidi ya mashambulizi ya mbu waharibifu. Kwa ajili hiyo majimoto hujulikana kama rafiki wa mkulima.

No comments:

Post a Comment

HI.............